Wednesday, December 28, 2011

Tatizo la Mafuta Tanzania

Bado ninajiuliza hili tatizo la upatikanaji wa mafuta Tanzania, ni tatizo la kweli au ni janja tu ya wanaojishughulisha na biashara ya mafuta kunufaika zaidi? 
  
Kwa nini matatizo yawe yanatokea katika vipindi ambapo watu ndio wanahitaji mafuta kwa wingi, na kwa nini linakuja pale bei ya EWURA inaposhuka tu. 
 
Bado najiuliza, mbona siku za nyuma tatizo hili lilikuwa halitokei? 
 
Kila la heri katika maandalizi ya mwaka mpya wa 2012!!!!

Friday, December 2, 2011

Waziri Mkuu wa Zimbabwe Tsvangirai Aachana na mke Mpya Baada ya Siku 12 tu

Waziri mkuu wa Zimbabwe, Morgan Tsvangirai, ameachana na mkewe ambaye ni mfanyabiashara tajiri nchini Zimbabwe Bi Lorcadia Karimatsenga Tembo mwenye miaka 39. 
 
Anadai chanzo ni kuingiliwa na vyombo vya usalama na kujaribu kumchafua kisiasa! Pia, anamshuku mkewe kuwa alikuwa anashirikiana na wana usalama ili kupanga njama za kumharibia kisiasa, kwani... at mkewe alikwenda kwa wazazi wake(Mke) bila kumtaarifu Waziri Mkuu (Mume). Hivyo kutokana na hayo, uhusiano wote umevurugika na hauwezi kusuluhishwa tena. 
  
Inadaiwa alikuwa amekwishalipa dola za kimarekani 36,000 na ng'ombe 10 kama mahali, lakini kwa kuvunja ndoa hii imebidi alipe dola 10,000 kama fidia kwani mke wake huyo alikuwa tayari ni mjamzito na alikuwa na watoto mapacha.

Pata habari kwa kimombo kwenye link hii

Thursday, December 1, 2011

Tujiepushe Na Maambukizi ya UKIMWILeo ni siku ya UKIMWI Duniani.
Tunakumbushana tu kujiepusha na vitendo au vyanzo vinavyoweza kuendeleza kueneza UKIMWI Duniani. 
  
Take Care for yourself and your loved ones!  

Monday, November 28, 2011

Hapa Hakuna Soko kwa Madaktari wa Kuremba na Dawa za Kichina

Si kila aliye nayo ni ya asili.  
  
Wafanyabiashara wamegundua au wamebuni makalio ya bandia yanayotengenezwa kiwandani na ya kuyauza kwa akina dada na akina mama wanaotaka kuonekana ya kuwa na wao wamejazia. 
  
Pichani dada wa ..... akijaribu na kupima muonekano wake huku akijiangalia kwenye kioo. 
  
Dunia hii ni ya ajabu, wale walionayo wanatamani yapungue, na wale wasio nayo wanafanya kila juhudi ili wayapate.

Kazi ya Mungu haina Makosa!

Thursday, October 27, 2011

MAANDAMANO YA KUPINGA SERIKALI KUILIPA DOWANS Sh. BILIONI 111

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI:

Novemba, 2010 Mahakama ya usuluhishi ya kimataifa ilitoa tuzo dhidi ya Tanesco kuilipa Dowans shillingi billion 94. Jambo hili liliibua hisia na hasira miongoni mwa wananchi kwa kulalamika na kupinga ulipaji huo wa fedha za umma kwa kampuni tata - kutokana na taarifa za kamati teule ya Bunge.

Baada ya tuzo hiyo watu binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali na mawakili wa Tanesco walipinga mahakama kuu kusajili tuzo hiyo. October 2011 Mahakama kuu ilitoa uamuzi wa kusajili tuzo hiyo na kuamuru Tanesco ilipe shillingi billion 94 na asilimia 7.5 ya gharama hizo. Hata hivyo kabla ya usajili wa tuzo hiyo, Dowans iliuza mitambo husika kwa kampuni ya Symbion Powers kinyume cha taratibu kwa kuwa kulikuwa na amri ya mahakama ya kuacha hali ya mitambo ibaki kama ilivyo. Cha kushangaza ni jinsi ambavyo Serikali ilikuwa mstari wa mbele katika kuingia mkataba wa uzalishaji wa umeme na Symbion Powers kwa gharama ya watanzania hali ikijua mitambo hiyo iko kwenye mgogoro uliopo mahakamani.
Kwa kuzingatia haya, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kwa kushirikiana na Asasi kadhaa za Kiraia na Wanaharakati wa Haki za binadamu tulitoa tamko tarehe 11 Oktoba 2011 kuitaka serikali kuchukua hatua ikiwa ni sehemu ya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa bila mafanikio.

Kwa kuwa serikali imeamua kudharau maoni yetu, na kwa kuwa kuna kila dalili kwa serikali kuilipa Dowans fedha za wananchi, sisi, asasi za kiraia, vyama vya wafanyakazi, serikali wakilishi za wanafunzi na raia wa kawaida wa Dar es salaam tunaitisha maandamano kwa uratibu wa kituo cha Sheria na Haki za Binadamu siku ya Jumamosi tarehe 29/10/2011. Kwa hapa Dar es salaam, maandamano yataanzia Ubungo, mbele ya zilipo ofisi za Makao makuu ya TANESCO hadi Viwanja vya Jangwani kuanzia saa 2:30 asubuhi.

Maandamano haya yanalenga kuitaka serikali kufanya yafuatayo:-

Kutokuilipa kabisa Dowans kwa kutumia hela za walipa kodi wa Tanzania.

Itoe maelezo ya kina kwanini ilipuuza ushauri wa kisheria wa kuvunja mkataba na Richmond toka awali kwani kwa mujibu wa washauri wa kimarekani Hunton & Williams LLP wakati Tanesco inaingia mkataba na Richmond Dev’t Co. Kampuni hiyo haikuwa imeshasajiliwa achilia mbali kuwa haikuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu yake chini ya mkataba huo.

Itekeleze kwa dhati maazimio 23 yaliyotolewa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania juu ya mlolongo mzima unaopelekea mpaka sasa tutakiwe kulipa bilioni 111. Kwa kufanya hili Serikali pia ituthibitishie kuwa itaacha kabisa kukikosea heshima chombo ambacho ni kisemaji na wakilishi cha wananchi kupitia wabunge.

Kama sheria za kimataifa zinatubana kulipa deni hili basi malipo haya yafanyike kwa kuuza mali za wale waliotusababishia kadhia hii na kwamba malipo ya kuilipa dowans yafanyike pale tu serikali itakuwa imeshawachukulia hatua kali wahusika wa kadhia hii. Umma ni lazima ujiridhishe kwa kuona hatua hizo zinachukuliwa.

Kuchukuwa hatua ya kinidhamu kwa wale wote walioshiriki katika kuingiza serikali katika mkataba huu hata mawakili waliotoa ushauri huu.

Serikali ipeleke Bungeni muswada wa utaratibu mzuri na sahihi wa kushirikisha wananchi na hata wabunge katika kuingia mikataba ya kimataifa na serikali ili kuepusha hali kama hii kutokea.

Kwa hiyo tunatoa wito kwa watanzania wote tuadhimishe kumbukumbu ya miaka 12 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa kutenda yafuatayo:-

Tujitokeze kwenye maandamano ya amani na kupinga ufisadi na malipo ya kifisadi ya Dowans siku ya Jumamosi, tarehe 29 Oktoba 2011.

Kuvaa nguo za maombolezo, nyeusi, kama ishara ya maombolezo tukikumbuka msimamo wake wa kupinga ufisadi na matumizi mabaya ya rasilimali za taifa,

Tuzitumie siku za ibada za Ijumaa, Jumamosi na Jumapili zote ndani ya muda huu, kumuomba Mungu atujalie Uzalendo na Ujasiri wa kuitetea nchi yetu, kama alivyofanya Mwalimu Nyerere,

Kuwasiliana na wanaharakati nchi nzima mahali walipo, ili kupanga na kuandaa mahali pa kukutania siku ya maandamano haya ya amani.
Mwisho, tunaomba walipa kodi (wananchi) wote ambao hawajapendezwa na mlolongo huu unaopelekea ulipaji wa deni hilo la Dowans na ufisadi mwingine wote kuwa na uthubutu na kujitokeza kwa wingi kusimamia kile ambacho wanaona ni haki na stahili ya wananchi wote na taifa letu kwa ujumla.

Thursday, September 22, 2011

Ujumbe Kupitia Katika Mavazi

Bada ya likizo ndefu, bado natafakari picha hii pamoja na ujumbe wake!

Nimeitoa kwa Allen Phillip

Wednesday, July 13, 2011

Hotuba ya Rostam Aziz kujiuzulu Ubunge na Ujumbe wa NEC

Hotuba ya Rostam Aziz kwa wazee wa Igunga kama ilivyotangazwa na TBC:


WAZEE wangu, kwanza kabisa kabla ya kueleza kile ambacho kimenisukuma kuzungumza nanyi leo, napenda kuanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kufikia siku hii ambayo inatukutanisha waja wake.
 
Wazee wangu wa Igunga, baada ya kufanya hivyo napenda pia kutumia fursa hii kuwashukuru ninyi nyote mmoja mmoja na katika umoja wenu kwa kuitikia wito wangu, kijana wenu, niliyewaomba nije nizungumze nanyi siku hii ya leo.
 
Nafanya hivyo nikitambua vyema kwamba, kama si nyinyi wazee wangu na wengine wengi ambao hatuko nao hapa leo kwa sababu mbalimbali, ambao mmekuwa na imani kubwa nami nisingeweza kufikia hapa nilipofika sasa.
 
Wazee wangu, waasisi wa taifa letu walitufundisha kutambua na kuheshimu ukweli kwamba; ‘Uongozi ni Dhamana’ dhana ambayo kila ninapokaa na kutafakari huwa inanirejesha nyuma na kukumbuka jinsi nyinyi mlivyokaa katika umoja wenu na kuniteua mimi, miongoni mwa vijana wenu wengi, kuwa mwakilishi wa Jimbo la Igunga tangu mwaka 1994.
Katika kipindi hicho chote cha utumishi wangu, nyinyi wazee wangu mmekuwa mhimili muhimu ambao umeniwezesha kutimiza wajibu wangu kwa bidii kubwa, maarifa na nidhamu ya hali ya juu nikitambua namna ambavyo mmekuwa na imani kubwa juu yangu.
 
Ari na moyo wa imani, ushirikiano na mshikamano ambao wazee wangu mmekuwa nao kwangu ndiyo ambao kwa kiwango kikubwa umetuwezesha kufanya kazi kwa pamoja, tukishinda changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikilikabili jimbo letu katika kipindi chote ambacho mmeendelea kuniamini kuwa mbunge wenu kwa miaka 18 sasa.
Wakati nikitambua na kuheshimu ukweli kwamba katika kipindi chote cha ubunge wangu mmekuwa na imani kubwa nami na kuniunga mkono kwa dhati, naamini kwamba kwa upande wangu pia nimejitahidi kwa kadiri nilivyoweza, kutimiza matarajio ya wananchi wa Igunga.
  
Miongoni mwa mafanikio makubwa tuliyoyafikia kupitia ushirikiano wetu na uongozi wa pamoja ni kwamba, mwaka 1994 Igunga ilikuwa ni wilaya ya mwisho kwa maendeleo mkoani Tabora lakini leo ndiyo ya kwanza, taa za barabarani, bima ya afya kwa kila kaya, zahanati kila kijiji na shule nyingi kuliko idadi ya kata zilizomo kwenye wilaya.
 
Wazee wangu, nayasema haya nikitambua kwamba, kama ilivyo katika maeneo mbalimbali hapa nchini, mafanikio makubwa tuliyoyapata katika nyanja za elimu, afya, makaazi bora na kilimo katika kipindi chote ambacho mmendelea kuniamini kuwa mbunge wenu kwa miaka 18 sasa.
 
Wakati nikitambua na kuheshimu ukweli kwamba katika kipindi chote cha ubunge wangu mmekuwa na imani kubwa nami na kuniunga mkono kwa dhati, naamini kwamba kwa upande wangu pia nimejitahidi kwa kadiri nilivyoweza, kutimiza matarajio ya wananchi wa Igunga.
 
Wazee wangu, nayasema haya nikitambua kwamba, kama ilivyo katika maeneo mbalimbali hapa nchini, mafanikio makubwa tuliyoyapata katika nyanja za elimu, afya, makaazi bora na kilimo katika kipindi hicho chote hayajaweza kumaliza changamoto zote za maendeleo ambazo zinatukabili.
 
Wazee wangu, ingawa nimekuwa na kawaida ya kukutana na kuzungumza nanyi mara kwa mara, mmoja mmoja na wakati mwingine katika umoja wenu, wito wangu wa leo una makusudi ambayo kwa kiwango kikubwa ni tofauti na yale ambayo tumeyazoea.
  
Japokuwa ujumbe ninaotaka kuzungumza nanyi wazee wangu, si mgeni sana masikioni mwenu, tofauti ya leo na mikutano yetu mingine iliyopita ni uamuzi ambao nimekusudia kuufanya na ambao nitayatangaza muda mfupi ujao.
 
YATOKANAYO
 
Wazee wangu, naamini mmekuwa mkifuatilia kwa karibu hali ya siasa nchini na hususani afya ya kisiasa na matukio mengine ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho mimi ni mwanachama wake na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) nikiuwakilisha Mkoa wetu wa Tabora.
 
Naamini kwamba katika kufuatilia kwenu mtakuwa mmebaini kuwapo kwa matukio ambayo kwa namna moja au nyingine yamekuwa yakitokea huku yakiligusa jina langu na wakati fulani nafasi yangu kama kiongozi wa chama hicho.
 
Wazee wangu, nayasema hayo kwa sababu mara kwa mara ninapokutana nanyi nikiwa katika ziara zangu jimboni na wakati mwingine mnapowasiliana nami kwa njia mbalimbali mmekuwa mkionesha kuguswa kushitushwa na kutaka kujua kulikoni kuhusu mambo hayo yanayotokea.
 
Mimi, kama mnavyonijua nyote, ni mtu muwazi na mkweli. Siku zote nimekuwa mwepesi sana wa kuwaeleza kuhusu kila kinachotokea ili kuwaondoa hofu na wakati huo huo kuwahakikishia kwamba masuala yasiyo na msingi hususani yale yanayogusa siasa za kitaifa hayawezi kutuondoa katika mstari sahihi wa kuwahudumia wananchi wa Igunga, mkiwamo nyinyi wazee wangu ambao mmeniamini na kunituma kuwawakilisha.
 
Nyinyi wenyewe ni mashahidi wazuri kwamba tangu matukio yanayogusa jina langu yaanze kutokea miezi michache tu baada ya Serikali ya Awamu ya Nne inayoongozwa na Rais Jakaya Kikweti kuingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 2005, tumekuwa tukiyapuuza na tukaendelea kufanya kazi pamoja kwa bidii.
 
Bado naamini na nitaendelea kuamini kwamba tulifanya uamuzi sahihi wa kuyapuuza matukio hayo kwani mbali ya kuendelea kutimiza malengo mbalimbali yaliyokuwamo katika Ilani yetu ya Uchaguzi ya CCM, pia mliendelea kuniamini kwa nafasi yangu ya kuwa mwakilishi wenu bungeni na hata mkaniruhusu nibebe jukumu jingine kubwa la kuwa Mjumbe wa NEC ninayewakilisha mkoa wetu wa kihistoria wa Tabora.
 
Wazee wangu, nyinyi ndiyo watu mnaolifahamu vyema jimbo letu la Igunga na hakika nyinyi ni sehemu muhimu ya watu wanaojua historia ya kisiasa ya Mkoa wa Tabora kwa miaka mingi hata kabla ya kuja kwa mfumo wa vyama vingi hapa nchini.
 
Hakuna shaka hata kidogo kwamba, Tabora ni kitovu hasa cha uasisi wa siasa za vyama vingi hapa nchini. Ni wazi kwamba huwezi ukazungumzia chimbuko la vyama vya upinzani tunavyoviona hapa nchini leo pasipo kugusa mkoa huu ambao umekuwa chimbuko la wanasiasa wenye mizizi hapa na nchini kwa ujumla.
 
Majina ya wanasiasa wa aina ya wazee wetu, hayati Chifu Said Abdallah Fundikira na Christopher Kassanga Tumbo, Kasela Bantu (Mungu awalaze mahala pema peponi), James Mapalala, Profesa Ibrahim Lipumba na mengi mengine yana mizizi yao katika Mkoa wetu wa Tabora.
 
Kutokana na ukweli huo basi ni wazi kwamba, nikiwa Mbunge wa Igunga kwa vipindi vinne mfululizo na wakati huo huo nikiwa Mjumbe wa NEC kwa vipindi vitatu mfululizo, moja ya kazi ambazo nimezifanya kwa uaminifu na kwa bidii kubwa huku nikiungwa mkono na kushirikiana nanyi ni ile ya kuhakikisha kwamba mkoa huu pamoja na kuwa kitovu cha upinzani unaendelea kubakia kuwa ngome muhimu ya kisiasa ya CCM.
 
Si vibaya tukakumbushana kwamba, wakati nachaguliwa kuwa mjumbe wa NEC wa Mkoa mwaka 1997, jimbo moja katika mkoa wetu lilikuwa likishikiliwa na upinzani. Leo hii Tabora ni mkoa pekee miongoni mwa mikoa iliyotuzunguka ambao haukupoteza jimbo hata moja kwenda upinzani katika Uchaguzi Mkuu wa 2010. Mafanikio haya tuliyafikia kwa pamoja kutokana na ushirikiano wenu wazee wangu.
  
Wazee wangu, Waswahili wanasema usione vyaelea, vimeundwa. Kazi ya kuijenga CCM katika mazingira yenye mizizi hasa ya upinzani nikiwa mbunge na hususani M-NEC kutoka Mkoa wa Tabora haijapata kuwa rahisi na itaendelea kuwa ngumu na ambayo mapambano yake ni makali sana.
  
Wazee wangu, kwa namna ya pekee kabisa napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru nyinyi wazee wangu wa Igunga na wananchi wenzangu wote wa Mkoa wa Tabora kwa kushikamana na kuifanya kazi hiyo kwa bidii, uaminifu na mafanikio makubwa.
 
Matunda ya kazi hiyo kubwa yanaonekana. Pamoja na kuwa kitovu cha kihistoria cha siasa za upinzani, Tabora ndiyo mkoa pekee katika eneo hili ambao unaongozwa na wabunge wote kutoka CCM baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na hata kabla ya hapo.
 
Kwa sababu hiyo basi, wazee wangu, sote katika umoja wetu ukiacha mafanikio makubwa tuliyopata katika jimbo na Wilaya yetu ya Igunga, tunayo mambo mengine ya msingi ya kujivunia. Kwa moyo wa dhati na kwa unyenyekevu mkubwa napenda kuwapongeza kwa namna mlivyojitoa kukipigania na kukitetea chama chetu kwa ari na nguvu ya kipekee.
 
KUJIVUA GAMBA
 
Wazee wangu, chama chetu chini ya uongozi wa Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete kimeamua kwa kauli na nia moja kujitathmini na kufanya mabadiliko makubwa ya kimfumo yenye lengo la kukiwezesha kiendelee kubakia chama kinachoaminiwa na kuungwa mkono na Watanzania walio wengi
 
Dhamira ya mwelekeo huo wa kufanya mabadiliko ya ndani ya chama chetu ilitangazwa rasmi na Mwenyekiti wetu Rais Kikwete wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 34 ya kuzaliwa kwa CCM, mjini Dodoma.
  
Katika hotuba yake hiyo, Rais Kikwete aliyafananisha mabadiliko hayo na tabia ya kawaida na ya asili ya nyoka na wanyama wengine kadhaa ya ‘Kujivua Gamba’.
 
Wazee wangu hatua ya kwanza ya utekelezaji wa azimio hilo na mwelekeo huo sahihi ilifanyika mjini Dodoma wakati wa kikao cha Kamati Kuu ya Taifa ya CCM ambacho mimi nilikuwa mjumbe wake.
  
Wakati wa kikao hicho, wajumbe wote wa Kamati Kuu na wale wa Sekretarieti ya chama chetu wa wakati huo kwa kauli moja tulikubaliana kujiuzulu, lengo likiwa ni kumpa Mwenyekiti wetu fursa nzuri ya kufanya mabadiliko ya uongozi yatakayotoa nafasi ya kupata mwelekeo mpya wa Chama.
 
Wazee wangu, tulifanya hivyo tukionesha kuunga mkono kwa asilimia 100 kile ambacho bado naendelea kuamini kuwa ni mawazo sahihi na yenye mwelekeo thabiti ya Mwenyekiti wetu ambayo kwa kiwango kikubwa yalikuwa yakiakisi matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa urais, ubunge na udiwani wa Oktoba mwaka jana.
  
Niliseme kwa maneno machache tu hili. Ingawa ni kweli kwamba Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana umekirudisha madarakani chama chetu kwa kukipa ushindi mkubwa katika uchaguzi wa urais, ubunge na udiwani kwa Tanzania Bara na Zanzibar, kiwango cha ushindi tulichopata kimeonyesha waziwazi dalili za wananchi kupunguza imani yao kwetu kuilinganisha na ilivyokuwa mwaka 2005.
  
Tungekuwa ni chama cha siasa cha ovyo iwapo tungepuuza kupungua kwa kura za rais kutoka zaidi ya asilimia 80 tulizopata mwaka 2005 hadi kufikia aislimia 61 mwaka jana kiwango ambacho ni pungufu kwa asilimia 20 ya kura katika kipindi cha miaka mitano tu, hasa ikizingatia ukweli kwamba mgombea urais ni mtu yule yule.
 
Tungekuwa ni chama cha siasa kilichokosa umakini iwapo tungekaa pasipo kuchukua hatua zozote za kujiimarisha baada ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu kuonesha wazi kukua kwa upinzani ambao umeongeza idadi ya wabunge na madiwani katika pande zote mbili za muungano.
 
Matokeo hayo ya uchaguzi ambayo hapana shaka yamekitikisa chama chetu yalitukumbusha wasia ambao tuliachiwa na Baba wa Taifa aliyesema; ‘Bila ya CCM Madhubuti Nchi Yetu Itayumba’.
  
Wazee wangu, kwa sababu ya kutambua ukweli kwamba hakuna haki isiyo na wajibu kama nilivyosema awali, mimi na wenzangu tuliokuwa katika Kamati Kuu tuliona ulazima, haja na umuhimu wa kukubali kwa kauli moja wito wa kututaka tujiuzulu ikiwa ni hatua moja ya kujipanga na kukijenga upya chama chetu.
  
KUJIVUA GAMBA KWAPOTOSHWA
 
Wazee wangu, kilichotokea baada ya kujiuzulu kwetu kila aliye ndani na nje ya chama chetu amekisikia na anakifahamu. Chama kilipata safu mpya ya uongozi iliyotokana na kuundwa kwa Sekretarieti inayoongozwa na Katibu Mkuu wetu mpya, Mhe. Wilson Mukama, na Kamati Kuu iliyokuwa na sura tofauti na ile ya awali.
 
Wakati tukitafakari na kuangalia mustakabali mpya wa kisiasa ndani ya chama chetu, ghafla yalianza kutokea mambo ambayo chokochoko zake zilianza kusikika tangu tukiwa ndani ya Kamati Kuu ambayo ilijiuzulu baadaye.
  
Mara tu baada ya kumalizika kwa kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ambacho kilichagua wajumbe wapya wa Kamati Kuu na kuidhinisha uundwaji wa Sekretarieti mpya, dhana ya kujivua gamba ambayo naamini Mwenyekiti wetu aliianzisha kwa nia njema ilianza kuenezwa ikichukua tafsiri na mwelekeo tofauti na ule wa awali.
  
Wajumbe wawili wa Sekretarieti, Naibu Katibu Mkuu (Tanzania Bara), Mhe. John Chiligati, na Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi, Mhe. Nape Nnauye, walisikika wakitangaza kwamba Halmashauri Kuu ya Taifa ilikuwa imefikia uamuzi wa kuwapa siku tisini wale walioitwa watuhumiwa wanaokabiliwa na tuhuma za ufisadi ndani ya chama kujitoa katika nafasi zao za uongozi vinginevyo watafukuzwa na chama.
  
Wazee wangu, baada ya kushinikizwa sana na vyombo vya habari wawataje kwa majina wanasiasa waliokuwa wakituhumiwa kwa ufisadi ambao ni wajumbe wa NEC na ambao wanapaswa kujiuzulu nyadhifa zao, wajumbe hao wa Sekretarieti walikwenda mbele zaidi.
  
Baada ya awali kuwaeleza waandishi wa habari kwamba majina ya watuhumiwa hao yalikuwa yakifahamika kutokana na kuhusishwa katika kashfa tofauti kama zile za Richmond, EPA na ununuzi wa rada, mwishoni viongozi hao walikaririwa wakiyataja majina ya wanasiasa watatu kuwa ndiyo ambao walikuwa wakilengwa na maamuzi hayo.
 
Wazee wangu, nilishangazwa na kushitushwa na namna porojo na fitina za kisiasa zilivyofinyangwa kwa mara nyingine tena baada ya kusikia jina la mbunge wenu ambaye ni mimi, likitajwa kuwa miongoni mwa yale matatu ya viongozi waliokuwa wakitakiwa eti kupima wenyewe na kisha kuchukua uamuzi wa kujiuzulu nafasi zao za uongozi ndani ya NEC katika kipindi cha siku tisini.
 
Niliseme hili mapema. Mshangao na mshituko wangu haukusababishwa na kutajwa kwa jina langu, la hasha, bali namna uamuzi halisi wa NEC na hususani dhana nzima ya ‘kujivua gamba’ ilivyoweza kupindishwa na wajanja wachache na kisha kuendeshwa kwa maslahi binafsi ya kikundi fulani cha watu.
 
Pili, nilishangazwa na kushitushwa na hatua ya viongozi wa chama changu ambacho nimekitumikia kwa bidii na uaminifu mkubwa kufanya juhudi kubwa hata kukivisha kikao kitukufu cha NEC uamuzi ambao msingi wa hoja zake ni vita vya kimakundi ya kisiasa yaliyo ndani ya CCM kwa upande mmoja na propaganda za vyama vya siasa vya upinzani na vyombo vya habari kwa upande mwingine.
  
Tatu, nilishangazwa na kushitushwa na ujasiri ambao umekuwa ukioneshwa na baadhi ya viongozi wetu wapya wa Sekretarieti wanaolitaja jina langu na kulihusisha na kile wanachokiita ufisadi ambao hata ukweli wa kimazingira na kihistoria ukiachilia mbali ushahidi wa wazi umeshathibitisha kwamba ni porojo za kisiasa zilizotokana na makovu na matarajio ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 na ule ujao wa 2015.
  
Wazee wangu, nyinyi ni mashahidi kwamba, mbali ya mimi mwenyewe kujitokeza kupitia vyombo vya habari na kueleza wazi kwamba sijapata kujihusisha katika vitendo vyovyote vya ukiukwaji wa maadili ya uongozi au vya rushwa, hakuna ushahidi wowote uliotolewa unaonihusisha na kashfa yoyote miongoni mwa zile zilizotajwa.
 
Wazee wangu, ni wazi kwamba kama chama chenye siasa chenye dhamana ya kuwaoongoza Watanzania kutoka katika lindi la ufukara, maradhi, matatizo ya makaazi na mengineyo siku zote tunapaswa kuwa makini katika kuhakikisha kwamba changamoto za kuwaongoza na kuwakomboa wananchi waliotupa dhamana hazitikiswi na mawimbi ya matakwa ya nyakati ama ya vyombo vya habari au wapinzani wetu wa kisiasa walio nje ya CCM.
 
Ni kwa sababu ya kulitambua hilo na hasa kuyatambua madhara yanayoweza kukipata chama chetu na nchi yetu iwapo tutaendekeza siasa za kupakana matope pasipo na sababu za msingi, kuchafuana kusikokoma na kulipizana kisasi ndiyo maana nimeona nitumie fursa hii kuzungumza nanyi wazee wangu ili kuweka kumbukumbu sahihi.
  
MAAMUZI YANGU
  
Wazee wangu, nimetafakari sana na kimsingi nimefikia hatua ya kupima yale ambayo yamekuwa yakisemwa na kuandikwa juu yangu na ambayo kwa mtazamo wangu unaoungwa mkono na wanafamilia yangu, marafiki zangu na washirika wangu wa kibiashara walio ndani na nje ya nchi, naona umefika wakati muafaka wa kuchukua hatua.
  
Kwa sababu ya kutambua uzito wa hatua ninazokusudia kuzichukua, niliona halitakuwa jambo la hekima hata kidogo iwapo ningefanya hivyo pahala pengine popote bali hapa Igunga mbele ya nyie wazee wangu.
Baada ya kukaa na wanafamilia yangu, marafiki na washirika wangu wa kibiashara niliona halitakuwa jambo la busara hata kidogo kuendelea kuvutana na viongozi wa chama changu na wanachama wenzangu wa CCM katika mambo ambayo yanaweza kumalizwa kwa njia muafaka.
 
Wazee wangu, sina budi niwaeleze kwamba, mbali ya athari za kisiasa na kifamilia, vita vya ovyo vya kisiasa kama hivi tunavyoviendesha na kuviendeleza ndani ya CCM na ndani ya nchi yetu huwa vina athari kubwa katika ulimwengu wa kibiashara. Athari kama hizo za kibiashara huingia ndani zaidi kuliko vichwa vya habari vya magazeti vinavyolenga kuchafuana, na athari hizo huwa kubwa zaidi kwa mtu kama mimi kwa sababu tofauti na wengine wengi hapa nchini, mimi ni mfanyabiashara wa kimataifa.
  
Katika ulimwengu wa kibiashara wa leo, vita hivi ambavyo vinaweza kuonekana kuwa ni vidogo tu vyenye malengo ya kuchafuana kisiasa, vinakuwa na athari kubwa katika uhusiano wa kibiashara kuliko hata wale wasioelewa wanavyoweza kukadiria. Ndiyo maana nimeona ni afadhali sasa niwape nafasi wale wanaoendesha siasa hizi uchwara na zisizo na tija waendelee na siasa zao hizo ambazo kwa bahati mbaya kwao, mimi sina muda nazo na siwezi kuwa sehemu yake. Na mimi kwa upande wangu niendelee na maisha yangu.  
  
Kutokana na ukweli huo na sababu zote hizo basi, kwa moyo wa dhati na kwa nia thabiti, hatua ya kwanza niliyoiona kuwa ninapaswa kuichukua ilikuwa ni hii ya kuitikia wito unaotokana na msukumo wa ndani ya nafsi yangu wa kuamua kukomesha kabisa malumbano na mivutano isiyo na manufaa kwangu binafsi, kwa viongozi wa chama changu na chama chenyewe.
Msukumo huo si mwingine bali ni ule wa kuamua kuachia nafasi zangu zote za uongozi ndani ya chama, nikianzia na ile ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa nikiuwakilisha Mkoa wa Tabora na hii ya ubunge wa Igunga ambazo kama si kwa baraka za chama changu nisingelikuwa nazo.
Napenda kuliweka hili sawa sawa. Uamuzi wangu wa kuachia nafasi zangu zote za uongozi nilizopata kwa tiketi ya CCM haukutokana na wala haumaanishi kukubaliana na shinikizo lililopotoshwa kuhusu azma ya utekelezaji wa dhana ya kujivua gamba, la hasha, bali dhamira ya dhati ya kuachana na siasa hizi uchwara (gutter politics) na kutumia muda wangu kushughulika na biashara zangu.

Aidha, nimefikia uamuzi huo lengo likiwa ni kuwajengea heshima na imani machoni mwa wanachama na wananchi wengine, viongozi wangu ambao naamini baada ya mimi kujitoa watapata fursa ya kutafakari upya changamoto nyingine mbadala zinazowakabili ambazo msingi wake ni dhamana kubwa walizo nazo za kukiongoza chama chetu na nchi yetu kupitia Serikali yake.
Wakati nachukua uamuzi huu, natambua vyema kwamba, watatokea watu ndani ya chama chetu na nje ambao watafanya kila juhudi kupotosha au kupindisha ukweli kuhusu hatima yangu ya kisiasa baada ya kujiweka kando na kujipa mimi mwenyewe na chama changu fursa ya kutafakari kwa kina majaaliwa yangu na ya nchi yangu katika siku zijazo.
Nafanya hivyo nikiwa na imani thabiti kwamba, uamuzi wangu huu, hususani ule wa kuachia nafasi yangu ya ubunge, yatakipa fursa nyingine CCM ya kuendelea kuliongoza jimbo letu la Igunga katika kipindi cha miaka minne ijayo kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Kwa upande mwingine, uamuzi wangu huu naona ni fursa kwa viongozi wa Chama changu cha CCM kutafakari na kuamua njia wanayoiona wao ni sahihi kuichukua kwa hatima na mustakabali wa chama chetu na ambayo wanaamini itakipa nguvu mpya ya kisiasa dhidi ya vyama vya upinzani.
Sambamba na hilo, ninayo imani thabiti kwamba, uamuzi wangu wa kubakia kuwa mwanachama wa kawaida na mtiifu wa CCM utakuwa chachu kwa chama changu na kwa Serikali yake kuwatumikia wananchi kwa Ari Zaidi, Kasi Zaidi na Nguvu Zaidi.
Mwisho kabisa, nikimalizia naomba nitumie fursa hii kutoa heshima za pekee kwa Rais Jakaya Kikwete kwa kazi kubwa aliyoifanyia na anayoendelea kuifanyia nchi yetu. Amefanya mengi na makubwa kuiendeleza nchi yetu na watu wake kuliko inavyothaminiwa na kufahamika. Kazi yake kubwa inashindwa kuthaminiwa na kufahamika kutokana na siasa chafu tunazoziendesha Tanzania. Wasia wangu kwa wanasiasa wenzangu, waandishi wa habari na Watanzania wenzangu kwa ujumla ni kuwa tunahitaji kuisaidia nchi yetu kwa kufanya siasa zenye mwelekeo wa kujenga ambazo ndiyo hasa zinapaswa kuwa siasa kwa maana halisi ya neno hilo.

Wazee wangu, baada ya maelezo hayo, nawashukuru sana kwa kunisikiliza na kunielewa.
Ahsanteni sana.

Nukuu kwa wavuti

Friday, July 8, 2011

Ngumi Za Mitaani!!!

Sijui ni ukosefu wa kazi, ulevi au kuchanganyikiwa akili.
Kama kawaida... wehu huu haukosi mashabiki, na watu wanaangalia tu

Saturday, June 11, 2011

Akina Dada, kuweni Waangalifu na Hawa Wehu!

Natanguliza kumradhi, hili tukio liliniogofya, nikaona nitoe onyo kwa wale wapenda kununua vitu vya barabarani. Jaribuni kuangalia mavazi ya muuzaji, japo inaweza isikinge kwa asilimia mia moja, lakini inaweza kukuepusheni na wasio nazo kama hawa!

Wednesday, June 1, 2011

Mambo ya Usawa wa Kijinsia


Piga kelele weeee, lakini.....

Wednesday, May 18, 2011

Williams, akina Dada wa Mfano


Ukakamavu wa mwili hauhitaji lelemama
Siri ya mafanikio ni kujituma na kufanya kazi kwa bidii
Siri ya ushindi ni kutekeleza kile unachokianmini kwa nguvu zako zote, akili zako zote na utashii wako wote bila kujali nani anasema nini


Siri ya akina dada hawa, ni kujituma na kufanya mchezo wa tenisi kama ndio ofisi ya maisha yao.

Mimi ni mpenzi na mfuasi mkubwa wa akina dada hawa

Thursday, April 21, 2011

Salamu za Juma Kuu na Pasaka

Wakati tunaendelea kuingojea sikuu ya Paska, tunapaswa kuwa wema kwa matendo na kukumbuka mateso ya yule watu wengi wanaomwaminiya ya kuwa alikubali kuteswa kwa ajili ya kiumbe binadamu. 
  
Wakati tunapotafakari picha hii na maajabu yake, basi tujiandae vyema kuupokea ufufko wake kwa matendo mema. 
 
Nawatakia kila la heri katika Ijumaa kuu, paska na jumatatu ya paska. 
  
Mbarikiwe sana

Friday, April 15, 2011

Maana ya Kujivua Gamba ni Nini?

Bado sijaelewa Dhana ya kujivua gamba.

Natazama... kama vile kupaka rangi nyumba bila kubadili chochote ndani, au kama vile nyoka anavyojivua gamba lake na kuondoka akiwa na kila kitu chake ikiwa ni pamoja na sumu, tabia, ukubwa, viungo na uwezo wake wa kizazi bila kubadili hata na jinsia.

Sasa wenzetu wamejivua gamba kivipi?

Mh! Nawatakia kila la heri na mafanikio, yote iwe kwa mema ya Tanzania na watu wake!

Monday, March 28, 2011

Have a Blessed Week!

For those who never had a glimpse of enjoyable weekend..
I just say ...... "After long and tiring weekend, may Almight God bless you for the whole of this week"
For those who are Christian believers.... I wish you the best and great humiliations ... during the lent period.

Have my blessings too!
Hata kikombe cha babu kinaaminika kuponya :-)

Thursday, March 24, 2011

Kuwa Mwangalifu Katika Ujana wako

Fiona Walker bado anajutia picha hii aliyopigwa mwaka 1976 akiwa bado ni kijana wakati huo akiwa na miaka 18 tu.  
Alikubali kupiga picha hiyo kumfurahisha mpenzi wake wa kiume ambaye alikuwa na tamaa ya kuwa mpiga picha maarufu.
Ilibidi aazime nguo na reki ya mchezo wa tenisi ili aonekane kama kweli alikuwa mchezaji mahili.     
    
Rafiki yake wa kiume aliweza kupata pauni kama laki mbili na nusu kwa kuruhusu kuuzwa kwa picha hiyo ambayo ilitolewa nakala kama milioni 2 baada ya kuonekana ilikuwa maarufu sana.  
  
Sasa hivi Fiona akiiona picha hii, anajuta na kusema kama angejua, katu asingekubali kupiga picha hiyo.  
  
Soma habari hii hapa

Monday, March 21, 2011

Tanzania: Chama Tawala ni kipi?

Naomba kusaidiwa kwenye utata huu.
Nifahamuvyo mimi, ni kuwa chama tawala ni kile kinachoshikilia dola, kwa maana ya kwamba ndicho kinachotoa kiongozi mkuu mwenye mamlaka ya serikali. Kwa maana nyingine ndio kiongozi wa kiserikali wa nchi hiyo. Ambaye anafanya kazi kwa mujibu wa sheria na katiba.
Hata kwenye nchi zinazo ongozwa kifalme (na kimalkia pia).
Vyama vya upinzani vina wajibu mmoja mkuu, nao ni kukisoa chama tawala pale kinapo endesha mambo ndivyo sivyo....

Kwa Tanzania mimi inanikanganya pale ninapojua ya kuwa chama hiki
ndicho chenye hatamu na ndicho chama tawala. Kimekuwa mstari wa mbele katika kujikita uongozini kwa juhudi zote kama vile kusukuma greda kwa kutumia fito.

Lakini kuna chama hiki

Kimekuwa kikishutumiwa sana na chama kileee juu ya kuwa kinataka kuleta uvunjifu wa amani kwa kuwaeleza watanzania waliolala usingizi mkubwa ya kuwa wananyonywa na kupelekwa pabaya. Na kuwa serikali yao haina jipya la kuwaletea kimaendeleo baada ya miaka 50 ya kuwa madarakani, hivyo waamke na kuchagua chama kitakacholeta maendeleo. Mimi nahisi huo ndio ukweli na maana ya upinzani. Kukosoa chama tawala pale kinapokosea.

Sasa huyu ndugu

naye anakuja juu na kumkashifu mpinzani wa serikali. Huyu ndugu anadai tena ati Chama chenye mamlaka ya wananchi kinataka kupinduliwa na chama kingine kwa kuwaamsha waliolala usingizi, ati wakiamka kwa ghafla watakuwa na hasira na mtawala wao kwa kugutuka kuwa walipokuwa wamelala, walikuwa wanapigwa bakora sana kama vile hawana akili nzuri..
Huyu ndugu kaungana na mwingine ambaye ana bendera ya bluu ambayo haipatikani mitandaoni na kumshambulia huyo anayekuja kwa nguvu za uma. Naye anadai mwenye dola anataka kupinduliwa kwa staili ya kuwaamsha watu wajue ya kuwa wanatembea bila nguo barabarani.
Sasa hapo ninachanganyikiwa, kwani sijui chama tawala ni nyundo au ni antenna.
Kama wewe unajua kisayansi, basi nielezee!!
Angalizo: Mimi sio mwanasiasa, ila ni mpenda maendeleo na ukweli


Thursday, March 10, 2011

Umakini wa Watanzania!


Waziri wa nishati na madini, Mhesh Ngeleja, wa tatu kutoka kushoto akisikiliza kwa makini hoja katika mkutano mmojawapo wa kimataifa.

Kulia kwake yupo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mh. Kikwete.

Picha kutoka kwa Mnyonge Mnyongeni....

Thursday, March 3, 2011

Uteuzi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa waishtua Rwanda

Rais Sarkozy amefanya uteuzi mpya wa waziri wa mambo ya nje na kumteua Allain Juppe.

Juppe alikuwa na wadhifa huo huo wakati wa mauaji ya kimbari yaliyoikumba Rwanda mwaka 1994 na inasemekana alikuwa anaiunga mkono kwa nguvu serikali iliyokuwa madarakani Rwanda wakati wa mauaji ya watutsi.
Alidumu katika wadhifa huo hadi mwaka 1995.

Waziri wa mambo ya nje wa Rwanda, Bibi Mushikiwabo, ameonyesha wasiwasi na kutofurahishwa na uteuzi huo ukuzingatia ya kuwa Rwanda na Ufaransa zimefufua mahusiano chini ya miaka 2 iliyopita, baada ya serikali ya Rais Kagame kuisusia Ufaransa kwa kile kilichokuwa kinaelezwa ya kuwa Ufaransa ilihusika moja kwa moja na uchochezi wa mauaji ya Kimbari ya watutsi, na hii ilipelekea Rwanda kubadili hata na lugha rasmi ya matumizi na kujiunga na jumuiya ya madola na kuanza kuzungumza na kufundisha shuleni kiingereza badala ya kifaransa.

Kumekuwa na wasiwasi ya kuwa watu watatoneshwa vidonda vya mauaji ya 1994 kwa uwepo wa waziri huyu kwenye wizara ile ile ambayo iliacha watu takribani milioni moja wakiuwawa kwa visasi.

Wednesday, February 16, 2011

Je? Tutafika Kweli??!!!!


Hizi picha nimezitoa kwenye blogu mbalimbali.
Tafakari... Hapa tunahitaji kasi ya aina gani ili tujikwamue na matatizo haya


Tuesday, January 25, 2011

CCM si Shwari Hata Chembe?


Kuna fununu kuwa hali ya kifedha ndani ya chama cha mapinduzi aka CCM iko tete hasa baada ya kukumbwa na rungu la kupoteza nafasi nyingi za ubunge, na hivyo kupungua kwa kiasi kikubwa cha ruzuku ya kila mwezi.
Pia inasemekana inasakamwa na madeni katika uchaguzi uliopita na kufanya viongozi waanze kuhaha kuokoa jahazi. Inasemekana shinikizo la kujilipa kupitia Dowans ndio nia hasa ya kupata pesa kwa ajili ya kuendesha shughuli za chama, kulipa madeni na pia kukatia rufaa baadhi ya matokeo ya uchaguzi uliopita katika sehemu ambapo CCM iliangukia pua!
Pia inaaminika ya kuwa wabunge wengi wa CCM wakati wa uchaguzi walijigharimia wenyewe kwa ahadi kuwa watarejeshewa baada ya uchaguzi, kwani ruzuku za majimboni, zilielekezwa kwenye nguvu ya kugombea urais!! Lakini kutokana na kuanguka kusikotegemewa kwa CCM, hali imekuwa ni mbaya.
Pia kuna mnong'ono kuwa kuna baadhi ya makatibu na wenyeviti wa kata, na hata wilaya, malipo yameanza kuwa magumu, na kuna watu wanasingiziwa kukihujumu chama wakati wa uchaguzi ili wapate kisingizio cha kuwacheleweshea mishahara yao au hata kuwarusha!
Inasemekeana kuna wimbi la mgogoro litafumuka ndani ya kijani/njano hivi karibuni iwapo hali hii tete itaendelea, ndio maana wanahaha kulipa haraka Dowans.
Haya ni maono tu, usiulize ushahidi!!
Picha ya bendera mbinuko kutoka kwa Matukio Daima

Thursday, January 20, 2011

Jamani, Nipo

Wapendwa wangu!!!

Mwaka huu, sijui kwa sababu ulianza na 1.1.11 nami ilikuwa siku yangu ya kuzaliwa, basi sijui nilichanganyikiwa!!!

Magimbi na matembele naona yalikuwa yamenilevya, hata hivyo yote ni heri, mimi ni mzima na buheri wa afya.

Nina matumaini nanyi pia mu wazima kabisa.
Nawashukuru kwa uvumilivu wenu, na cha muhimu kupita mara kwa mara kusalimia nyumba iliyokuwa haina mwenyewe.

Mungu awabariki sana!!
Tupo pamoja