Thursday, November 25, 2010

Mtazamo wangu Katika Baraza Jipya la Mawaziri 2010

JK ametangaza baraza jipya la mawaziri.
Lina sura nyingi mpya, na watu wengi kama sio wote, hawajawahi kuhusishwa na tuhuma nzito au ufisadi.

Kuna mmoja au wawili, nyendo zao kimahusiano na wengine hazikuwa nzuri sana, na walikuwa ni watu wakati mwingine wa kuropoka na kudandia vitu, na hata kuwakejeli wafanya biashara maarufu walio safi.

Watu watahoji kwa nini JK ameweka wanawake wachache kuliko watu walivyotumainia?

Mimi kwangu hainikuni kichwa, kwani aliahidi kuweka watu wenye ufanisi, watakaondoa ukiritimba, wachapa kazi na walio karibu na wananchi wote wa Tanzania. Kwa maana nyingine maslahi ya Taifa mbele.

Dhana ya kuchagua wanawake tu mradi kufurahisha kundi la watu fulani hatupaswi kuliweka mbele, tunapenda pale ambapo mwanamke ana sifa sawa na mwanaume, basi hapo ndipo mwanamke atakapopendelewa, na sio hata yule aliye hoi na mbumbumbu wa kitu fulani basi na apewe nafasi ya uongozi eti kwa sababu tu ni mwanamke. Mambo yote haya yapo sambamba na kupiga vitu undugunaizesheni katika kazi.

Kama una rafiki au ndugu ambaye ni mchapa kazi na mwadilifu, kwa nini asipewe nafasi wakati sifa zote anazo. Mimi ninaamini ukiwa muadilifu, basi unatafuta na marafiki waadilifu, ukipata nafasi ya kuchagua wachapa kazi, basi kama rafiki yako ana uwezo naye anapewa nafasi. Kama ni goigoi, basi hana nafasi. Na hakuna atakayekulaumu kwa kumtupilia mbali.

Napenda wanawake tuchukue hii changamoto kwa hali ya uchanya, tusihoji kwa nini wanawake ni wachache, bali kwa nini tusijitahidi na sisi kupata nafasi hizo. Nina imani tunaweza kama tutajiamini na kuongeza bidii. Tusisubiri kila kitu kuamuliwa, halafu tunaenda kulalama pembeni bila kuongeza juhudi.

Sina budi kutoa pongezi hasa kwa baadhi ya mawaziri wanawake kama Prof Tibaijuka, Mama Kombani, Mary Nagu na wengineo huku nikiendelea kusubiri matunda ya baraza jipya la mawaziri kama kweli litatoa dira ya uelekeo wa CCM kwa miaka mingine 5, kwani kwa muda uliopita, tulitiwa kichefuchefu, tuna matumaini hatutatapishwa sasa.

God bless Tanzania

Friday, November 19, 2010

Kampeni za Uchaguzi 2015 Kumbe Zimesha Anza

Wakati watu wengine wanahangaika na kuona CHADEMA kitafanya nini kwenye bunge lijalo, kumbe kuna baadhi ya waheshimiwa wamekwisha anza kujipanga kwa ajili ya kugombea urais 2015.

Habari hizi ambazo bado zipo kwenye mvumo wa kichini chini zinadai kuna wanasiasa maarufu na wenye majina makubwa ambao wameshawahi kuwa mawaziri wameanza mkakati mkubwa wa kuhakikisha wanachaguliwa kuwa viongozi wa nchi.

Kati yao wapo waliowahi kuwa mawaziri na wakalazimika kujiuzuru nyadhifa zao kufuatia kashfa zilizowaandama ndani na nje ya bunge.

Yasemekana pia kuna aliyewahi kuwa waziri mkuu, na anaonekana amepania vilivyo, kwani alianza kampeni mapema hata kabla ya uchaguzi wa 2010 kufanyika. Na amekuwa hataki kujionyesha ya kuwa anawania kiti hicho, lakini ameshaunda kamati yake ya ushindi! Na anaendelea "kununua" watu ili wamuunge mkono wakati ukiwadia.
Habari hii inaweza kuwa uzushi, lakini mara nyingi kwa siasa zetu hizi chafu na safi, chochote kinawezekana.

Kwa mtazamo wetu, tunahisi wale wenye kashfa ambazo hazijafutika au kuamuliwa kihaki, wana nafasi ndogo ya kupenya ili wawanie uongozi hasa wa nchi kwa siku zijazo.

Tukumbuke kuchagua mbivu na si mbichi au pumba

Thursday, November 11, 2010

Uchaguzi wa Spika Tanzania... Ni Ujanja tu au?....

Inaelekea kuwa vurugu, mipasuko na vidonda vya uchaguzi bado havijapona!!

Suala la msukumo wa kumpata spika wa Bunge la Tanzania unaingia sura mpya mara baada ya CCM kuwachagua wanawake tu kushindanishwa,

Binafsi, nalipongeza suala hili, kwani inaonekana kama vile inajali wanawake, lakini unaweza kukuta ukweli ni kuwa wameona hao mafahali waliokuwa wanatonyana kwenye vyombo vya habari hawawezi kukaa zizi moja iwapo mmoja watampa nafasi ya kukaa juu ya mwingione, ndio maana wakateua wananwake tu! Kama misingi ilikuwa ni ya mtazamo huu, basi bado CCM hawakuwa na mpango wa kuteua wanawake, isipokuwa kuwageuza jamvi la kuficha uovu wao kwa kuwaendesha kwa remote :-(

Kuna wengine waliopendekezwa tulishawasahau kwenye nyanja za siasa... lakini mara wameibuka katika kugombea uspika....sasa hapo kweli sio kwamba wamepanga kwa makusudi mtu fulani kwa matakwa yao?

Saturday, November 6, 2010

Kikwete Aapishwa Kuwa Rais 2010 - 2015

HAYA. Mambo yanaelekea yamekwisha, leo JK ameapishwa baada ya kuchaguliwa na 27% ya watanzania waliojiandikisha kupiga kura, na 61% ya wale waliojitokeza kupiga kura!

Hapo hakuna cha kujivunia, ila kushukuru Mungu tu kuwa labda wale ambao hawakujitokeza wangepigia upinzani!

Nawapa pole wanafunzi wote wa vyuo, kwani hawakuweza kupiga kura baada ya serikali kuamua vyuo visifunguliwa hadi uchaguzi uishe ilhali wanafunzi wengi walijiandikisha wakati wakiwa chuoni. Nina hakika wengi walikuwa wanataka mabadiliko.

Ndio mwanzo huu, tunasubiri sasa mambo ya kukata rufaa na muda wa kuanza serikali mpya, tukiwa na matumaini kutakuwa na mabadiliko makubwa kiutendaji, na baadhi ya watu kupoteza ubunge wao kupitia mahakama.

Picha kutoka michuzi