Mfumo wa kisiasa Duniani na hasa katika nchi zinazoendelea ndio unaochangia kwa kiasi fulani kuendelea kuwafanya wanawake wawe katika hali duni.
Kilio cha wanawake wengi katika sehemu nilizopata kuzisikia leo, ni kule Uganda ambapo wanawake wamelalamika vifo kwa akina mama wajawazito vinazidi kuongezeka
Huko Kongo wamelalamika unyanyasaji na ubakaji
Dar es salaam wameonyesha wadi ya watoto wakiwa wamerundikwa kitanda kimoja na huku wazazi (akina mama) wanalala chini
Lakini nimeipenda changamoto ya Rais Kikwete aliyesema mabadiliko ya mwanamke yatatoka kwa mwanamke mwenyewe, na hiyo ndio falsafa amabayo mimi binafsi ninayoiamini.
Wiki kadhaa zilizopita nilikuwa nasoma utafiti mmoja uliofanyika huko Luanda, mji mkuu wa Angola kwenye kijarida kiitwacho HEALTH CARE FOR WOMEN INTERNATIONAL: Adaptation of health care seeking behaviour during child birth.
Habari niliyoikuta humo ilinifungua zaidi uelewa wangu. Kwani ilichambua kikamilifu kutoka kwa akina mama wenyewe sababu iliyokuwa inawafanya wasiende kujifunguia hospitali
Sababu zifuatazo ndio zilizotolewa:
- Walikuwa wakijisikia wageni na uoga hospitali tofauti na wanapokuwa nyumbani, kwani wengine walikuwa wametoka kwenye maeneo ya vita, na walikuwa na wasiwasi wa kuvamiwa tena wakiwa hospitali
- Gharama za hospitali zilikuwa ni kubwa na hazieleweki (labda hongo)
- Kulikuwa hakuna watu wa kukaa nao ambao wamewazoea kama wanapokuwa nyumbani ukizingatia na kauli za wauguzi na mlolongo mzima wa kulazwa
- Lugha chafu za wauguzi kwenye chumba cha leba, wakati mwingine wazazi watarajiwa kuzabwa makofi wakati wa uchungu
- Kufanyiwa upasuaji bila wazazi wenyewe kuelimishwa na wakati mwingine walikuwa wanaambiwa sababu ndogo tu
- Wale walikokuwa na historia ya kuzaa usiku tu walikuwa wanaogopa kwenda hospitali uchungu ukianza kwa kuogopa majambazi njiani.
- Kulazimishwa kukaa mkao fulani wakati wa kujifungua wakati wao wanapendelea mwingine
- kuongezwa njia wakati mtoto anatoka wakati wakunga wa jadi hawafanyi hivyo
- Kwa ujumla walikuwa wanapendelea nyumbani kwa sababu kuna watu wanaowajua karibu, na kuwafariji uchungu ukizidi, na pia wanakuwa na muhudumu muda wote tofauti na chumba cha leba.
Lakini pia kuna taarifa ya sehemu fulani nchini kwetu ya kuwa wakunga wa jadi huwalazimisha mabinti wakajifungulie nyumbani, na wakati wa ujauzito kuwapa mabinti dawa za kutapika ili watoto wasiwe wakubwa ili iwe rahisi kujifungulia nyumbani katoto kadogo!
Pia uhaba wa vifaa vya kujifungulia, huchangia wakina mama kwenda hospitali dakika za majeruhi kuepuka vifaa vyao kutumiwa na watu wengine, pia kukwepa kero za lugha chafu za manesi na kubanana kitanda kimoja huku kila mtu akiguna kivyake.
Tunajua umuhimu wa mzazi mtarajiwa, kwani anatarajiwa kuleta kiumbe hai kingine duniani. Mimi nafikiri tuchukue kumbukumbu hii ya siku ya wanawake kwa kuboresha eneo hili, kwani linachukua sehemu kubwa ya vifo ambavyo vinatokea kwa watu ambao sio wagonjwa (Kuwa na ujauzito sio ugonjwa).
2 comments:
Hongera wanawake wote Dunianai kwa siku hii.
Habari hii ni ya kusikitisha, na hata huko Uganda wanawake wamefanya maandamano kuonyesha hasira yao kutokana na vifo vya akina mama wajawazito tena wakiwa hospitali.
Tatizo kubwa kwetu siasa yetu inaangalia kufaidika kwa tumbo la mlafi mmoja bila kujali watu wengine huduma za afya wanazipataje.
Nakubalina nawe ya kuwa mjamzito si mgonjwa.
Together we can eliminate this problem.
Post a Comment