Wednesday, January 25, 2012

Mgogoro wa Wizara ya Afya na Madaktari!!!

Tanzania yetu ni nzuri sana. 
 
Viongozi wanajiamulia wanavyotaka wakitegemea walio chini yao kukaa kimya kama vile hawaoni wala hawasikii. 
Mtu akikunyima haki yako anataka ufunge domo lako. ati uking'aka kidogo, basi anatishia kukuumiza au kukutimulia mbali kama vile vumbi, na wala asitake kujua utaangukia wapi na nani utaenda kumchafua kwa kumuangukia, kwani umetimuliwa mahali na kufikishwa pengine pasipo matarajio yako. 
 
Huko unakotua, ukimuangukia mtu, anakukung'uta huku akitukana kama vile wewe ulipenda, au alifanya makusudi kuanguka mahali ulipoangukia. 
 
Ikiwa umeona umeumizwa kwa adhabu uliyopewa, ambayo hukustahili kuipata, bali yule aliyekupa adhabu hiyo ndio alitakaiwa kulaumiwa, basi yeye ndio anakuwa wa kwanza kwenda kulalama kwenye vyombo vinavyopaaza sauti ya kuwa anakushangaa kwa nini unapiga kelele wakati yeye hata hajakugusa!! Kama vile anawaowaambia ni majinga tu na ambayo hayaoni kitu!!. 
  
Vurugu hizo sasa zinakuwa za mafahari wawili, wao hawaumii kama vile nyasi zisizo na hatia, tena ambazo hupendwa sana na mafahari hao ili waweze kuishi, basi ndio wanazichakaza kwa mvutano wao, huku fahari mkubwa ambaye ndio mchokozi, akitaka kuonekana ndio mwema na anayejali uwepo wa nyasi wanazozikanyaga!!! 
  
Huku huyo fahari mkubwa akijua ya kuwa hata wakizichakaza hizo nyasi, yeye nyasi zake zipo ughaibuni, tena zinarutubishwa zaidi zikimsubiri yeye, na yule fahari mdogo hana zaidi ya kukubali kukanyagwa mabegani mwake, ili fahari mkubwa apande na kuingia kwenye pipa ili akale nyasi nzuri akimuacha fahari mdogo akilamba zilezile nyasi walizozikanyaga...... 
  
Ama kweli... huu mgogoro wa madaktari na wizara yao ukome. Wanaoumia ni wagonjwa!!!

Monday, January 2, 2012

Wayne Rooney Alimwa Faini ya Mshahara wake wa Wiki Nzima na Klabu Yake


Siri ya mafanikio katika jambo lolote, ni kuwa makini na nidhamu kwa kile unachokifanya.
Mafanikio katika kazi na michezo yote yanahitaji adabu kubwa kwa kufuatilia taratibu zilizopo, na katuika michezo ni kufuata maelekezo ya kocha. 
Kinyume cha hapo, kinaweza kukugharimu kitaaluma na kimaendeleo. 
 
Ndio maana Mkufunzi mkuu na meneja wa Manchester United Mhesh Alex Ferguson hakusita kuwachukulia hatua kali wachezaji wake watatu ambao ni Wayne Rooney, Darron Gibson na Jonny Evans ambao walitoka pamoja usiku kwenda kwenye klabu kula wakiambatana na mke wa Rooney kwenye siku ya kufungua zawadi (Boxing day) 
 
Adhabu hii ilikuja baada ya kuonekana ya kuwa wachezaji hawa hawakufanya vizuri katika mazoezi ya timu siku iliyofuata na hivyo meneja wao Ferguson kuudhika, na hivyo kutoa adhabu ya kukatwa mshahara wao wa wiki nzima (Wayne Rooney anapokea pauni za Kiingereza 250,000 kwa wiki, yaani zaidi ya TZS 600M), na pia kuondolewa kwenye kikosi kilichopambana na timu ya Blackburn, japo Man-U ilipata kichapo kutoka kwa timu iliyokuwa inashikilia mkia ya Blackburn. 
  
Hakukuwa na taarifa ya kuonyesha ya kuwa walikunywa pombe kupita kiasi wala kufanya tukio lolote la kutia fedheha, lakini adhabu ilikuja kama wembe mkali.
 
Mimi si mfuatiliaji sana wa mpira japo huwa napenda kuungalia, lakini msimamo mkali na adhabu ya kukata kipato cha mchezaji kwa asilimia 25 mara moja kwa kosa moja, inaonyesha jinsi gani watu wapo makini sana katika kuangalia na kulinda mafanikio ya kazi zao. 
  
Je, na sisi tupo tayari kuwa makini sana na kazi zetu? 
Nafikiri siri ya mafanikio ni kuwa makini katika kila tunalolitenda. 
 
Nawatakia juma jema lenye mafanikio 
  
Habari hii ipo BBC

Sunday, January 1, 2012

Tumeanza mwaka Mpya wa 2012

Ninamshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma kwa kunijalia kufanikiwa kuuona mwaka mpya wa 2012.  
Kila ninapoanza mwaka mpya, na ndipo ninaposheherekea siku yangu maalumu ya kuzaliwa. Kwa hiyo huwa nina furaha isiyo na kifani. 
 
Ninawatakia watu wote Heri ya mwaka mpya wa 2012.