Wednesday, January 25, 2012

Mgogoro wa Wizara ya Afya na Madaktari!!!

Tanzania yetu ni nzuri sana. 
 
Viongozi wanajiamulia wanavyotaka wakitegemea walio chini yao kukaa kimya kama vile hawaoni wala hawasikii. 
Mtu akikunyima haki yako anataka ufunge domo lako. ati uking'aka kidogo, basi anatishia kukuumiza au kukutimulia mbali kama vile vumbi, na wala asitake kujua utaangukia wapi na nani utaenda kumchafua kwa kumuangukia, kwani umetimuliwa mahali na kufikishwa pengine pasipo matarajio yako. 
 
Huko unakotua, ukimuangukia mtu, anakukung'uta huku akitukana kama vile wewe ulipenda, au alifanya makusudi kuanguka mahali ulipoangukia. 
 
Ikiwa umeona umeumizwa kwa adhabu uliyopewa, ambayo hukustahili kuipata, bali yule aliyekupa adhabu hiyo ndio alitakaiwa kulaumiwa, basi yeye ndio anakuwa wa kwanza kwenda kulalama kwenye vyombo vinavyopaaza sauti ya kuwa anakushangaa kwa nini unapiga kelele wakati yeye hata hajakugusa!! Kama vile anawaowaambia ni majinga tu na ambayo hayaoni kitu!!. 
  
Vurugu hizo sasa zinakuwa za mafahari wawili, wao hawaumii kama vile nyasi zisizo na hatia, tena ambazo hupendwa sana na mafahari hao ili waweze kuishi, basi ndio wanazichakaza kwa mvutano wao, huku fahari mkubwa ambaye ndio mchokozi, akitaka kuonekana ndio mwema na anayejali uwepo wa nyasi wanazozikanyaga!!! 
  
Huku huyo fahari mkubwa akijua ya kuwa hata wakizichakaza hizo nyasi, yeye nyasi zake zipo ughaibuni, tena zinarutubishwa zaidi zikimsubiri yeye, na yule fahari mdogo hana zaidi ya kukubali kukanyagwa mabegani mwake, ili fahari mkubwa apande na kuingia kwenye pipa ili akale nyasi nzuri akimuacha fahari mdogo akilamba zilezile nyasi walizozikanyaga...... 
  
Ama kweli... huu mgogoro wa madaktari na wizara yao ukome. Wanaoumia ni wagonjwa!!!

No comments: