Thursday, November 25, 2010

Mtazamo wangu Katika Baraza Jipya la Mawaziri 2010

JK ametangaza baraza jipya la mawaziri.
Lina sura nyingi mpya, na watu wengi kama sio wote, hawajawahi kuhusishwa na tuhuma nzito au ufisadi.

Kuna mmoja au wawili, nyendo zao kimahusiano na wengine hazikuwa nzuri sana, na walikuwa ni watu wakati mwingine wa kuropoka na kudandia vitu, na hata kuwakejeli wafanya biashara maarufu walio safi.

Watu watahoji kwa nini JK ameweka wanawake wachache kuliko watu walivyotumainia?

Mimi kwangu hainikuni kichwa, kwani aliahidi kuweka watu wenye ufanisi, watakaondoa ukiritimba, wachapa kazi na walio karibu na wananchi wote wa Tanzania. Kwa maana nyingine maslahi ya Taifa mbele.

Dhana ya kuchagua wanawake tu mradi kufurahisha kundi la watu fulani hatupaswi kuliweka mbele, tunapenda pale ambapo mwanamke ana sifa sawa na mwanaume, basi hapo ndipo mwanamke atakapopendelewa, na sio hata yule aliye hoi na mbumbumbu wa kitu fulani basi na apewe nafasi ya uongozi eti kwa sababu tu ni mwanamke. Mambo yote haya yapo sambamba na kupiga vitu undugunaizesheni katika kazi.

Kama una rafiki au ndugu ambaye ni mchapa kazi na mwadilifu, kwa nini asipewe nafasi wakati sifa zote anazo. Mimi ninaamini ukiwa muadilifu, basi unatafuta na marafiki waadilifu, ukipata nafasi ya kuchagua wachapa kazi, basi kama rafiki yako ana uwezo naye anapewa nafasi. Kama ni goigoi, basi hana nafasi. Na hakuna atakayekulaumu kwa kumtupilia mbali.

Napenda wanawake tuchukue hii changamoto kwa hali ya uchanya, tusihoji kwa nini wanawake ni wachache, bali kwa nini tusijitahidi na sisi kupata nafasi hizo. Nina imani tunaweza kama tutajiamini na kuongeza bidii. Tusisubiri kila kitu kuamuliwa, halafu tunaenda kulalama pembeni bila kuongeza juhudi.

Sina budi kutoa pongezi hasa kwa baadhi ya mawaziri wanawake kama Prof Tibaijuka, Mama Kombani, Mary Nagu na wengineo huku nikiendelea kusubiri matunda ya baraza jipya la mawaziri kama kweli litatoa dira ya uelekeo wa CCM kwa miaka mingine 5, kwani kwa muda uliopita, tulitiwa kichefuchefu, tuna matumaini hatutatapishwa sasa.

God bless Tanzania

4 comments:

Halil Mnzava said...

Sawa dada!yetu macho kuona utendaji wao.
Ubarikiwe!!

Mzee wa Changamoto said...

"Dhana ya kuchagua wanawake tu mradi kufurahisha kundi la watu fulani hatupaswi kuliweka mbele, tunapenda pale ambapo mwanamke ana sifa sawa na mwanaume, basi hapo ndipo mwanamke atakapopendelewa, na sio hata yule aliye hoi na mbumbumbu wa kitu fulani basi na apewe nafasi ya uongozi eti kwa sababu tu ni mwanamke."
Hapa umenena. Lakini kinachonipa shaka ni kama WANAWAKE 9 TU NDIO WENYE UWEZO WA KUFANYA KAZI? Yaani hata JK mwenyewe aliyekubali kuwa awamu ya kwanza aliitumia kujifunza, anategemea ni lini kinamama watajifunza (hasa kwa kuwa mfumo wetu haufunzi walio chini)?
Yaani kwa ujumla, wanawake wenye uwezo wa ki-utawala ni asilimia 18 tu (9 kugawa kwa 50 zidisha kwa 100).
Ni kweli?
Nadhani Kikwete alistahili kuweka bayana KAZI ZA KUFANYWA NA MAWAZIRI kisha kuweka MIKAKATI YA KUFUATA kisha tuone kama baraza hilo (hata kama lingekuwa la wanawake watupu) lingeshindwa kutuikisha "ng'ambo ya pili".
Tatizo ni kuwa wanategemea watu waongoze kwa akili zao bila muongozo, na ndio maana niliomba MAWAZIRI WATUELEZE WATAFANYA NINI, WATAFANYA VIPI NA KUFIKIA LINI (rejea http://changamotoyetu.blogspot.com/2010/11/nionavyo-mimimawaziri-waorodheshe.html)

emu-three said...

Kama alivyonena mzee wa changamoto, watupe ilani zao binafsi kama wizara, watafanya nini, ili iwepo hadharani, na sisi tuwe tunafuatilia ahadi zao, kwani wizara inayoshughulikia barabara, ina jukumu kubwa sana, kwani inagusa wanachi, na inachangia kiasi kikubwa kurudisha watu nyuma.
Pia mambo ya nishati hasa umeme, hili ni gonjwa sugu, Kama ingekuwa mimi ningepiga fagio la chuma, niwekwe wazalendo wenye uchungu na nchi yao. fikiria umeme unavyokatika sasa hivi mnategemea nini tufanye sisi wajasiriamali wadogowadogo ...

Upepo Mwanana said...

Suala la JK kuchagua watu 9 tu, duh, siwezi kulisema, nina imani wapo wengi zaidi ya hapo, labda kimkakati wake, si unajua alikuwa mjeshi zamani.....
Mimi navuta subira kwanza.